BAADHI YA MASWALI YAULIZWAYO MARA KWA MARA - KAWI YA KINUKLIA

BAADHI YA MASWALI YAULIZWAYO MARA KWA MARA - KAWI YA KINUKLIA

Ni kwa nini kenya inahitaji kawi ya kinuklia ?

Utoaji wa nguvu za umeme nchini Kenya kwa sasa ni wa takribani megawati 2300 .Kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Dira   2030 kunahitajika utoaji wa megawati zaidi za umeme hadi zaidi ya 16,000MW chini ya kipindi cha miongo miwili. Wakati vyanzo vyengine vya utoaji wa umeme vinapowekwa pamoja havifikii utaji unaokadiriwa kufikia 2030. Je, jawabu ni lipi? Bila shaka, kuna uhitaji wa utoaji waumeme kwa njia ya nuklia.

Vyanzo vya Kenya vya utoaji wa kawi ya umeme ni pamoja na utumiaji wa nishati ya mvuke, upepo, maji kwenye mabwawa na kutumia miale ya jua.

Makaa ya mawe na gesi yatajumuishwa katika mradi uliyoanzishwa September 2013, unaopania kuongeza kiwango cha stima kwa megawati alfu tano kufikia mwisho wa mwaka 2016. Nuklia nayo ikijumuishwa mwongo mmoja kuanzia sasa.

Vyanzo hivi vya kawi vitasaidia vyengine vilivyoko kuimarisha utoaji huo ili kustawisha viwanda, kubuni nafasi za kazi na utoaji bora wa bidhaa. Mipango kabambe kama vile kuwa na mfumo wa reli wa kutumia nguvu za umeme, Mji wa teknologia wa Konza, mpango wa uchukuzi wa LAPSSET utakaounganisha Lamu, Sudan ya Kusini na Ethiopia, pamoja na miradi kibao ambazo ni msingi wa ruwaza 2030 zinahitaji viwango vikubwa vya kawi.

Je umeme unaotokana na nguvu za ardhi na maji unatosha kwa utashi wa Kenya wa kawi hiyo?

 

Hapana. Kwa uchache Kenya inahitaji kuongeza uzalishaji wa stima hadi takriban megawati 16,000 kufikia mwaka wa 2030 ikilinganishwa na utoaji wa sasa wa kama megawati 1,700. Hata ikiwa Kenya itaweza kutumia nishati ya mvuke kwa ujumla, ikiwa ni wastani ya kati ya megawati 7000 na megawati 10,000, bado kuna nakisi kubwa ya kawi. Kwa hivyo mpango ulioratibiwa kutoa megawati 4000 kupitia kawi ya nuklia kufikia   mwaka wa 2030 ni mwafaka.

Na je kawi inayotokana na nguvu za upepo na jua?

Kawi hiyo ni moja ya mipango ya utoaji wa nguvu za umeme isiyokuwa ya gharama kubwa. Hata hivyo nishati hiyo haiwezi kukidhi mahitaji ya umeme katika viwanda vikubwa vikubwa kwa vile kiwango chake ni cha chini mno. Aidha, hupatikana tu kwa muda, ama jua linapochomoza au wakati kuna kasi ya juu ya upepo.

Na kuhusu usalama ?

Nguvu za kinuklia zinahitaji tahadhari ya hali ya juu. Misingi ya usalama ni muhimu na ni sharti yazingatiwe kwa umakini. Shirika la kimataifa la kawi ya kitonoradi (IAEA) lina miongozo thabiti kuzisaidia nchi zinazotoa kawi ya kinuklia. Kenya inaandaa misingi ya usimamizi bora huku usalama ukipewa kipaumbele.

Je kenya ina utaalamu unaohitajika ?

Serikali inatoa mafunzo kwa wanasayansi chipukizi wa Kenya katika fani zote zinazohusika na kawi hii ya kinuklia.

Tangia mwaka wa 2012, kadri wanafunzi 16 wamesomea shahada za uzamili katika sayansi ya kinuklia huko Korea Kusini. Sita kati yao walifuzu mwezi February 2014.

Wanafunzi wengine wanasomea shahada za uzamili katika chuo kikuu cha Nairobi katika kitivo cha Sayansi na Teknolojia ya Nuklia. Hatua hii itaimarishwa katika kipindi cha mwongo mmoja ujao ili kuhakikisha kwamba Kenya ina wataalamu wanaohitajika katika nyanja hii.

 

Je kenya itagharamia vipi mpango huu wa uzalishaji wa nguvu za umeme za kinuklia ?


Afua moja itakuwa ni kwa serikali kuugharamia mpango huu. Afua nyengine ni ya kupitia uwekezaji wa kibinafsi wa ujenzi wa kiwanda hicho na wafanyikazi wenye uzoefu na ujuzi. Na afua nyengine ni ya kutafuta usaidizi wa kifedha kwa njia ya mkopo.

Je kiwanda cha kinuklia cha kenya kitajengwa wapi ?


Utafiti unaofanywa unalenga kubaini eneo mwafaka za ujenzi wa viwanda vya kinuklia nchini Kenya. Ni mambo mengi yanayozingatiwa katika utafiti wa kisayansi. Maeneo yatakayopendekezwa kisha yatachunguzwa kitaalamu kwa kina na ukete. Baadhi ya maswala yanayozingatiwa ni mazingira, uwepo wa vyanzo vya maji, uwezekano wa kuathiriwa na mtetemeko wa ardhi, na pia umbali na sehemu ambapo kawi hiyo itatumika.

Ni manufaa gani itakayopatikana kwa gatuzi/kaunti kuwa mwenyeji wa kiwanda cha kuzalisha umeme wa nuklia ?

Manufaa ya kwanza kabisa ni mapato kutokana na bidhaa na huduma. Pia, kutakuwa na ajira wakati wa ujenzi wa kiwanda na hata litakapoanza kuzalisha umeme. Fauka ya hayo kutakuwa na manufaa ya uimarishaji wa muundo msingi kupitia ujenzi wa barabara na asasi za afya na za maslahi ya kijamii. Na si hayo tu, faida nyengine itakuwa ni upatikanaji wa nguvu za umeme kwa bei nafuu.

Baada ya kuvumbuliwa kwa mafuta ya petroli huko turkana, je kenya bado inahitaji kuendeleza mipango ya kuwa na kiwanda cha kinuklia ?


Ndio. Kuvumbuliwa kwa mafuta ya petroli ni muhimu sana kwa Kenya kwani kutawezesha nchi kupata fedha za kigeni kutokana na mauzo ya mafuta hayo. Mapato hayo yatawezesha uboreshaji ya miundo msingi. Uvumbuzi huo, ukiambatanishwa na ujenzi wa kiwanda cha kinuklia basi unapiga msasa uwezekano wa kutekelezwa kwa Dira 2030.

Ni nchi gani zilizo na viwanda ya kawi ya kinuklia ?

Ufaransa inatoa zaidi ya asili mia sabini na nane ya nguvu zake za umeme kutoka kwa nuklia. Lakini Marekani ndiyo inayotoa kiwango kikubwa zaidi cha umeme kutoka kwa nuklia ulimwenguni kote. Japan, Russia, Korea Kusini, Ujerumani, Ukraine, Canada, China, Uingereza, Uswidi, Uhispania, Ubelgiji, India, Jamhuri ya Czech, Finland, Bulgaria, Hungary, Brazil, Afrika Kusini, Slovakia, Mexico, Romania, Argentina, Pakistan, Slovenia na Uholanzi ni miongoni mwa nchi zengine zinazotumia teknologia ya nuklia kuzalisha nguvu za umeme.  

Ni nchi zipi za afrika zilizo na nguvu za kinuklia?

Afrika Kusini ina viwanda viwili vya utoaji wa umeme wa nuklia.   Kenya, Ghana, Nigeria, Misri, Cote d’Ivoire, Niger, Tanzania, Uganda na Tunisia ni miongoni mwa mataifa yaliyo mbioni kupanga mikakati kuwezesha utumiaji wa nuklia kuzalisha umeme.

Kinafanyaje kazi kiwanda cha kinuklia?

Viwanda vya kawi viwe ni vya makaa ya mawe, gesi ama nuklia, vinatumia mvuke kutengeza nguvu za umeme.   Vinafanya kazi kama birika kubwa lenye maji yanayochemka. Joto hilo hugeuza maji kuwa mvuke unaozungusha mitambo mikubwa ya kutoa nguvu za umeme. Tofauti ya pekee na viwanda vyengine ni kwamba viwanda vya nuklia vinatumia madini ya uranium kama chanzo cha joto.